×

Rais wa Zamani wa Korea Kusini Ahukumiwa Miaka 30 Jela

Rais wa zamani wa Korea Kusini, Yoon Suk-yeol.

Mahakama ya Seoul imemhukumu Rais wa zamani wa Korea Kusini, Yoon Suk-yeol, kifungo cha miaka 30 gerezani kufuatia tuhuma za kuhusika katika operesheni ya kijeshi iliyohusisha matumizi ya droni kuelekea Korea Kaskazini.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, operesheni hiyo ililenga kuchochea taharuki mpakani na kuandaa mazingira ya kutangaza sheria ya kijeshi mwaka 2024, hatua iliyosababisha mvutano mkubwa wa kisiasa na kijeshi kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini.

Inadaiwa kuwa droni hizo zilitumika pia kusambaza vijikaratasi vya propaganda ndani ya eneo la Korea Kaskazini, jambo lililoongeza zaidi hali ya sintofahamu katika mpaka wa nchi hizo mbili ambazo zimekuwa katika uhasama wa muda mrefu.

Mahakama hiyo imesema ushahidi uliowasilishwa ulionesha wazi kuwa hatua hizo zilihatarisha usalama wa taifa na kuvuruga utulivu wa kikanda, licha ya Yoon Suk-yeol kukanusha vikali kuhusika na kutoa maagizo ya operesheni hiyo.

Hukumu hiyo ni moja kati ya maamuzi makubwa zaidi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani, ambaye tayari alikuwa ameondolewa madarakani kupitia mchakato wa kikatiba ulioidhinishwa na Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini.

Kesi hiyo imezidi kuzua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi, huku wachambuzi wakisema inaweza kuathiri zaidi siasa za Korea Kusini na uhusiano wake na Korea Kaskazini katika siku zijazo.

Leave a Comment