
Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Musukuma amemwomba Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi kuchukua hatua dhidi ya kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali, ambazo amesema zinaweza kuchochea hisia za ubaguzi kati ya Uzanzibar na Utanganyika.
Akichangia Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 yenye thamani ya Shilingi trilioni 62.3, leo Jumanne Juni 16, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Musukuma amesema ni muhimu kulinda mshikamano wa kitaifa na kuepuka kauli zinazoweza kuleta mpasuko.
Amesema katika maeneo mbalimbali kama Geita ambako kuna shughuli za uchimbaji wa madini, Wazanzibari hufanya kazi na kuishi bila kubaguliwa, jambo linaloonesha kuwa Watanzania wanaishi kwa pamoja bila tofauti za kikanda.
Musukuma, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, amesisitiza kuwa kauli za kibaguzi kutoka kwa baadhi ya viongozi zinaweza kutafsiriwa kama msimamo wa Serikali, hivyo akapendekeza hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha mshikamano wa kitaifa unalindwa.
Kauli hiyo imeibua mjadala mpana ndani na nje ya Bunge kuhusu umuhimu wa viongozi kuwa makini na lugha wanazotumia katika kuzungumzia masuala ya muungano na utaifa.