×

Video: Polisi Wafunguka Sakata La Mbowe Kuvamiwa- Front Page

Msemaji wa jeshi hilo, SACP David Misime

Jeshi la Polisi Tanzania limezungumzia sakata la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kushambuliwa nyumbani kwake jijini Dodoma kwa kusema kwamba, hakuna mkanganyiko wowote uliotokea kuhusu suala hilo.

Hayo yamezungumzwa mapema hii leo na msemaji wa jeshi hilo, SACP David Misime alipokuwa akizungumza kwa njia ya simu kwenye kipindi cha Front Page kinachorushwa na +255GlobalRadio.

Misime aliyasema hayo mara baada ya mtangazaji wa kipindi hicho ambacho pia kilirushwa moja kwa moja na Global TV Online, Lucas Masungwa kumuuliza kuhusu mkanganyiko uliojitokeza baina yake na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto mara baada ya kutokea kwa tukio hilo.

“Hakuna mkanganyiko wa aina yoyote, tatizo la baadhi yetu Watanzania tunataka yale ambayo tunayafikiria sisi ndio yawe sahihi. Badala ya kuongozwa na ushahidi unaotokana kwenye eneo la tukio, unaotokana na watu walioshuhudia tukio au ushahidi wa kimazingira.

“Tunapenda kuhitimisha jambo fulani kulingana na mapenzi yetu binafsi ndio tatizo ambalo linaonekana. Alichozungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (Muroto) yeye alizungumza kilichoripotiwa kituoni. Kwamba yeye (Mbowe) amevamiwa, akashambuliwa, akakanyagwakanyagwa. Sio kwamba yeye alithibitisha.

“Alisema taarifa zake alizotoa ndizo alizozifikisha polisi na taarifa inavyofikishwa polisi tunaifanyia uchunguzi. Sasa mimi nilitoa taarifa yangu kulingana na uchunguzi unaondelea na bado kuna ushahidi mwingine mkubwa sana ambao tunaendelea nao kwa hiyo turudie tena kusema, Watanzania wasipende kukimbilia kutoa hitimisho badala ya kutegemea ushahidi uliopo,” alisema Misime.

Kauli aliyoitoa Misime ambayo ilitofautiana na Muroto ni hii hapa:
“Hakuna shahidi yeyote aliyesikia au kuona Mbowe akishambuliwa. Ilidaiwa alionekana ametoka kwa mzazi mwenzike Joyce Mukya (Mbunge wa Viti Maalum).”

Unaweza kuisikiliza +255GlobalRadio kwa kupakua App ya Global Publishers au kutembelea tovuti ya www.globalpublishers.co.tz kupata vipindi vingi vizuri.

Stori: Erick Evarist

 

 

Leave a Comment