
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani na Iran zimefikia makubaliano ya awali (memorandum of understanding) yanayosisitiza kuwa Iran haitakuwa na silaha za nyuklia.
Akizungumza katika mkutano wa G7 nchini Ufaransa, Trump alisema nakala ya makubaliano hayo itatolewa hadharani katika siku zijazo, na pia akapendekeza ipitiwe na Bunge la Marekani kwa mapitio rasmi.
Amesema mazungumzo hayo yameingia hatua ya pili, ambayo anaamini inaweza kuwa rahisi zaidi kuliko awali, huku akisisitiza kuwa Marekani haitowekeza fedha yoyote moja kwa moja nchini Iran.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema mazungumzo ya awamu mpya kati ya Marekani na Iran yanaweza kuanza Ijumaa, yakilenga kufikia makubaliano ya mwisho kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.
Makubaliano hayo ya awali pia yanahusisha suala la usalama wa Hormuz, ambapo pande zote zimeeleza matumaini ya kufungua njia hiyo muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani.
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema hakuna fedha zilizotolewa kwa Iran, na msaada wa kiuchumi utategemea hatua zitakazothibitishwa za Iran katika kupunguza na kudhibiti mpango wake wa urutubishaji wa uranium.
Mazungumzo haya yanaonekana kuwa hatua muhimu zaidi katika kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo mawili, huku masoko ya dunia yakipokea kwa tahadhari maendeleo hayo yanayoendelea.