ILIPOISHIA IJUMAA:
Nikaenda. Kilikuwa ghorofa ya kwanza. Nilipomaliza kupanda ngazi, nilianza kukitafuta chumba namba 35. Nikakiona. Nikaenda kubisha mlango.
Kitu kilichonishangaza ni kuwa licha ya kubisha mlango kwa sekunde kadhaa sikupata jibu. Nikaujaribu mlango ambao ulifunguka, nikaingia ndani. Smith mwenyewe hakuwemo chumbani ila niliona suti yake kwenye kitanda. Sikujua alikuwa ametoka au amekwenda wapi.
Nikajaribu kufungua mlango wa bafuni. Nilichokiona kwenye macho yangu kilinipasua moyo na kunifanya niache mdomo wazi kwa mshtuko.
SASA ENDELEA…
Nilimuona Smith amesimama akioga. Alikuwa mtupu kama alivyozaliwa. Kwa vile alielekea upande uliokuwa na mlango wa bafu nilimuona waziwazi.
Kitu cha kwanza kilichonistaabisha ni ule weupe uliokuwa kwenye ngozi yake, haukuwa weupe wa kawaida na haukuwa weupe niliozoea kumuona nao ninapokutana naye. Ulikuwa weupe uliopitiliza! Isitoshe ngozi yake iliota manyoya marefu kama ngozi ya mnyama. Manyoya hayo yalimuota mwili mzima kwenye miguu, kwenye mikono, kwenye shingo na kwenye kifua na tumbo ndiyo kulikuwa na msitu kabisa!
Yalikuwa manyoya meupe kama yaliyopakwa rangi. Kwa vile manyoya hayo yalikuwa yameingia maji yalikuwa yamelala kwenye ngozi na kuonekana kama ya nyani mzee aliyenyeshewa na mvua.
Kioja hakikuwa hicho tu, macho yake ndiyo yaliyotisha zaidi. Yalikuwa kama ya paka mwitu yakiwa na mboni zilizounda mstari mwembamba wa kijivu halafu yalitoa nuru kali kama yalikuwa yanawaka.
Bado. Kucha zake za miguu na mikono zilikuwa ndefu kama kucha za kubandika. Yaani hazikuwa tofauti na mnyama!
Niliogopa. Nikajiambia, kumbe huyu mzungu yuko hivi! Huyu ni jini si binadamu!
Nikaufunga ule mlango haraka na kutetea maisha yangu. Nilikimbilia kwenye mlango wa chumbani nikaufungua na kutoka mbio!
Nilishuka ngazi mbilimbili hadi nikafika chini. Nikatoka nje ya ile hoteli huku nikishukuru Mungu kuwa nimenusurika.
“Yule jini angenifyonza damu leo!” nikajiambia.
Macho yangu yalikuwa yakiangaza huku na kule kutafuta teksi.
Kwa vile nilikuwa natetemeka kwa hofu, hadi makalio yangu yalikuwa yanacheza. Magoti nayo yalikuwa yakininyong’onyea, yaani nisingeweza tena kutembea kwa miguu. Ningeanguka tu.
Nikaiona teksi. Lakini wakati naifuata nilisikia nikiitwa nyuma yangu.
“Enjo!”
Nilipogeuka nyuma nikamuona yule mzungu amenifuata nje ya hoteli, sasa akionekana wa kawaida tu.
“Enjo hebu simama, unakwenda wapi sasa?” Smith akaniuliza.
Nilijuta kugeuka nyuma. Kwa kweli sasa nilikuwa namuogopa yule mzungu. Nikageuza uso wangu haraka kuelekea mbele. Nilikuwa nimeshaifikia ile teksi. Dereva alishanifungulia mlango wa nyuma.
“Ingia twende!” akaniambia.
Nikajipakia huku nikitetemeka. Mwili ulikuwa umeishiwa nguvu kabisa.
Wakati nafunga mlango nilimuona Smith naye akifuata teksi.
“Nikupeleke wapi?” Dereva wa teksi niliyojipakia akaniuliza.
“Nipeleke Sinza.”
Teksi ikaondoka.
Nilipomtazama tena yule mzungu kwenye kioo nilimuona akipanda teksi.
“Anakwenda wapi?” nikajiuliza kwa hofu.
Baada ya muda kidogo niligundua kuwa alikuwa ananifuata mimi. Teksi aliyopanda ilikuwa nyuma ya ile teksi niliyopakiwa.
“Mama yangu…leo nimekwisha!” nikajiambia na kutoa simu yangu.
Nikampigia dada huku jicho langu likiwa kwenye teksi aliyopanda Smith.
Dada akapokea simu.
“Dada kumbe yule mzungu niliyekuelezea mchana ni jini, nimemfuata hapa hotelini nikamuona bafuni anaoga lakini ana umbile la kijini. Nimemkimbia kwa teksi lakini ananifuata nyuma kwa teksi nyingine. Mwambie shemeji anifuate haraka…” Nilimwambia dada kwa sauti ya mtu aliyepatwa na hofu kiasi cha kukaribia kulia.
Tayari dada akawa amepatwa na wasiwasi. Akaniuliza tulikuwa wapi. Nikamwambia.
“Mzungushezungushe tunawafuata,” dada akaniambia na kukata simu.
Nikafungua pochi yangu na kutoa noti tatu za shilingi elfu kumikumi, nikampa yule dereva.
“Shika hii pesa, nataka uichenge hii teksi iliyo nyuma yetu kabla hatujaenda Sinza,” nikamwambia dereva huyo kisha nikamuuliza.
“Utaweza?”
Dereva aliitazama teksi hiyo kwenye kioo akaniambia.
“Kazi ndogo tu.”
Alitia gea. Teksi ikafyatuka na kuanza mbio. Alikata kona kadhaa kuikwepa teksi hiyo lakini baada ya muda kidogo tukaiona tena nyuma yetu. Tumbo lilikuwa likiniunguruma kwa kujua siku ile ulikuwa ndiyo mwisho wangu. Haja kubwa ilikuwa karibu kunitoka. Nilikuwa nimelikaza tumbo nisiadhirike.
“Huyu jamaa hachengeki,” dereva wa teksi akaniambia.
Kabla sijamjibu kitu dada akanipigia simu na kuniuliza tuko katika barabara gani. Nikamtajia.
Baada ya muda kidogo nikaona gari la shemeji limetokeza mbele yetu.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.
Lilitaka kutupita nikatoa mkono kwenye dirisha na kulipungia huku nikipiga kelele.
“Shemeji! Shemeji!”
Gari hilo llikasimama pembeni mwa barabara.
“Dereva rudi nyuma ulifuate lile gari,” nikamwambia dereva wa teksi huku nikijisikia ahueni kuliona gari hilo.
Dereva wa teksi akapunguza mwendo na kukata kona. Akalifuata gari hilo la shemeji lililokuwa limesimama.
Ile teksi iliyokuwa nyuma yetu ilipita moja kwa moja na kwenda kusimama mbele.
Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.