KAMA ni haki, wahusika wa elimu nchini walipaswa kushtakiwa kwenye mahakama za kimataifa za makosa ya kiutu kwa kusimamia utoaji elimu mbovu wenye sura ya kudhalilisha.
Nisamehewe kama nimetumia maneno makali; lakini usipuuzwe wajibu wangu kwa jamii kuisemea kupitia kalamu yangu juu ya yale ambayo serikali inawakosea wananchi walioiweka madarakani.
Miaka miwili iliyopita, niliwahi kuikosoa serikali juu ya mfumo wake wa utoaji elimu isiyokuwa na usawa. Nilimweleza waziri mwenye dhamana ya elimu wakati ule, Shukuru Kawambwa kuwa anafanya dhambi kubwa kuwashindanisha kwenye mtihani mmoja wanafunzi wanaofundishwa vizuri na wale wasiofundishwa.
Kwa dhati ya moyo wangu nilisema kosa hilo linatosha kumuweka kwenye kundi la wenye dhambi. Maana si sawa kwa mazingira yalivyo kwenye shule za vijijini kwa wanafunzi wanaohitimu huko kufanya mtihani mmoja na wanafunzi wanaosoma shule za mijini zenye vifaa na walimu wa kutosha.
Shule za vijijini hakuna umeme, mazingira ya kufundishia mabovu, walimu wa kutosha ‘ziro’, vifaa vya kufundishia ‘magumashi’ tupu!
Wanafunzi wa vijijini wanakoishi wananchi wengi hawajui chai na mkate, wanasoma na njaa na wakati mwingine wanalazimika kutembea umbali mrefu kuzifuata shule, wakitoka nyumba za nyasi wanakolala kwenye vumbi na kusomea shule za nyasi kwa kukaa kwenye vumbi.
Katika hali ya utu, heshima na kuthaminiwa; wanafunzi wanaohitimu kwenye mazingira haya ya vijijini wanawezaje kuitwa wamefeli kwa kulinganishwa na wale wa mijini wanaotoka nyumbani kwa gari huku wamekumbatia keki kuelekea kwenye shule zinazofundishwa na walimu wa kutosha wenye vifaa vya kisasa vya kufundishia?
Sina hakika kama ukosoaji wangu ulimfikia Waziri Kawambwa, maana ni hulka ya watawala wengi kujiona wanajua kila kitu kiasi cha kutosikia ushauri mwingine. Naam, nadhani alinipuuza.
Kwa sasa ninachoshukuru, Kawambwa amewambwa kwa kung’olewa wadhifa wake na elimu aliyokuwa anaisimamia imekosolewa na waziri mpya, Prof. Joyce Ndalichako.
Mwanzo wa utendaji kazi wake, Prof. Ndalichako ameonesha dhamira ya kufufua elimu iliyokufa hapa nchini lakini pamoja na nia hiyo nzuri, tafsiri ya matamshi yake ya hivi karibuni ya kukusudia kuchukua hatua ya kupangua mrundikano wa walimu kwenye baadhi ya shule na kuwapeleka kwenye shule zenye uhaba wa watoa elimu, imemuweka mahali pa mtu kusubiri utafiti; kutafiti anachokijua ili achukue hatua za utekelezaji.
Prof. Ndalichako hana asichokijua juu ya upungufu wa walimu kwa baadhi ya shule hasa vijijini; anajua kuna shule zenye walimu watatu wanaofundisha wanafunzi zaidi ya 200.
Ndalichako huyu anafahamu kabisa walimu wengi wamerundikana mijini kama sehemu ya kukwepa kufundisha shule za vijijini zenye mazingira magumu.
Waziri wa elimu anaelewa kuna sekondari za jamii zinazoitwa za kata, masomo ya sayansi na hesabu hayana walimu, wanafunzi wanawekwa kwenye mazingira ya kufeli si kwa sababu hawana akili bali hawafundishwi.
Kwa mazingira haya, serikali Kama ilivyokuwa kwa Kawambwa, namwambia waziri wa elimu wa sasa, Prof. Ndalichako, lazima achukue hatua za kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu kwa wanafunzi hapa nchini inakuwa kwa wote, asipofanya hivyo anachuma dhambi na dhambi hiyo itamuweka pabaya.
Salaam kwako Prof. Ndalichako, tena wasalaam, ama baada ya salamu… matatizo ya elimu yetu hapa nchini unayoyajua usisubiri ripoti za uchunguzi, chukua hatua ili usiwe mtu mwenye maneno mengi bila vitendo. Wizara ya elimu uliyopewa iko mahututi, ukizubaa itakufia mikononi mwako.
huwa inapata wapi ujasiri wa kuwatangaza wanafunzi wa aina hii kuwa wamefeli? Serikali hii kwa nini isiwe na uungwana wa kujitangaza yenyewe kuwa imewafelisha wanafunzi ili kuwapa nafuu katika maumivu ya kufeli? Nashauri kama muungwana!