
Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, ameivunja Serikali yake baada ya kubaini kuwa imeshindwa kutekeleza majukumu yake na kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa hatua hiyo imewalazimu viongozi wote wa Serikali kujiuzulu.
Serikali hiyo ilitimiza chini ya asilimia 10 ya malengo yake, licha ya kupewa dhamana ya kuongoza taifa hilo mwaka 2024.
Makamu wa Rais, Teodoro Nguema Obiang Mangue, amesema kuwa Waziri Mkuu aliwasilisha rasmi barua ya kujiuzulu kwa niaba ya Mawaziri wote, kwa kuzingatia kanuni ya uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Amesisitiza kuwa kiwango cha utekelezaji kilichofikiwa hakikuendana na matarajio wala ahadi zilizotolewa kwa wananchi.
Aidha, kwa mujibu wa chama tawala cha Democratic Party of Equatorial Guinea (PDGE), Rais Obiang hajaridhishwa na utendaji wa Serikali hiyo kutokana na tuhuma za rushwa, matumizi mabaya ya rasilimali za umma kwa manufaa binafsi, pamoja na kusuasua kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi, Equatorial Guinea bado inakabiliwa na changamoto za kiuchumi na umaskini unaowaathiri wananchi wengi.
Uchumi wa taifa hilo umeendelea kudorora katika miaka ya karibuni kutokana na kupungua kwa uzalishaji na mahitaji ya mafuta duniani, hali ambayo imeongeza shinikizo kwa Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato na kukuza uchumi wake.