×

Rais wa Bolivia Atangaza Hali ya Dharura Kufuatia Maandamano na Mzozo wa Kiuchumi

Rais wa Bolivia, Rodrigo Paz, ametangaza hali ya dharura nchini humo huku maandamano makubwa yanayoikumba nchi hiyo ya Amerika Kusini yakiendelea kwa zaidi ya siku 50.

Tangazo hilo linatoa mamlaka ya kupeleka wanajeshi zaidi katika maeneo mbalimbali ili kurejesha utulivu na kuondoa vizuizi vya barabarani vilivyowekwa na waandamanaji.

Makundi mengi ya waandamanaji yanadaiwa kumuunga mkono rais wa zamani wa Bolivia, Evo Morales, na yamekuwa yakifunga barabara kuu nchini kote. Hatua hiyo imesababisha kusimama kwa usafirishaji wa bidhaa muhimu kama chakula, mafuta na dawa, huku mji mkuu wa utawala wa nchi hiyo, La Paz, ukiwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi.

Mzozo huo ulianza baada ya serikali ya Paz kuondoa ghafla ruzuku ya mafuta iliyokuwepo kwa muda mrefu, wakati taifa hilo likikabiliwa na kushuka kwa thamani ya sarafu yake na kuanza mazungumzo ya kifedha na International Monetary Fund (IMF).

Licha ya serikali kupunguza bei ya mafuta na kusitisha baadhi ya mageuzi ya mfumo wa ardhi yaliyopingwa na wananchi, maandamano yaliendelea kushika kasi. Vyama vya wafanyakazi vimeendelea kudai nyongeza ya mishahara na kumtaka rais huyo kujiuzulu.

Tangazo la hali ya dharura limekuja saa chache baada ya Paz kusaini makubaliano na chama kikuu cha wafanyakazi nchini Bolivia (COB), yaliyolenga kupunguza mvutano wa kisiasa na kijamii.

Akizungumza baada ya kutangaza hatua hiyo, Paz alisema lengo ni kurejesha utulivu, kulinda usalama wa wananchi na kuhakikisha bidhaa muhimu zinaendelea kuwafikia raia. Pia alionya kuwa watu watakaoendelea kuvuruga amani na shughuli za usafirishaji watakabiliwa na hatua kali za kisheria.

Leave a Comment