×

Algeria Yaibukia Fifa, Yadai Messi Alistahili Kadi Nyekundu, Yataja Dhuluma ya Waamuzi

Shirikisho la Soka la Algeria limelalamikia kile lilichokiita dhuluma ya uamuzi wa waamuzi kwa FIFA kufuatia kipigo cha mabao 4-0 walichopata dhidi ya Argentina katika mchezo wao wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026.

Malalamiko hayo yamejikita zaidi kwenye tukio la dakika ya 30 ambapo nahodha wa Argentina, Lionel Messi, alimkanyaga beki wa Algeria, Aïssa Mandi, kwa viatu kutoka nyuma, lakini hakupewa hata kadi ya njano.

Kwa mujibu wa chanzo kutoka Shirikisho la Soka la Algeria, tukio hilo lilistahili adhabu ya kadi nyekundu, huku pia wakieleza kuwa kulikuwa na matukio mengine mawili ya matumizi ya viwiko yaliyopaswa kupelekea wachezaji wa Argentina kutolewa nje ya uwanja.

Licha ya malalamiko hayo, Messi aliendelea kung’ara katika mchezo huo kwa kufunga mabao matatu (hat-trick), na kufikisha jumla ya mabao 16 katika historia ya Kombe la Dunia, akilingana na rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Ujerumani, Miroslav Klose.

Algeria imesisitiza kuwa haikanushi ubora wa Argentina kama mabingwa watetezi wa dunia, lakini haiwezi kunyamazia maamuzi ambayo inaamini yalikuwa ya upendeleo.

“Tunakubali Argentina ni timu imara, lakini hatuwezi kukaa kimya mbele ya dhuluma. Kulikuwa na matukio matatu yaliyo wazi kabisa na VAR haikuingilia kati,” kilisema chanzo hicho.

Sasa Algeria inajiandaa kwa mchezo wake wa pili wa Kundi J dhidi ya Jordan Jumatatu kabla ya kumalizia hatua ya makundi dhidi ya Austria Juni 27, huku ikisaka kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya pili katika historia yake ya Kombe la Dunia.

Leave a Comment