
WASANII wakongwe wa muziki wa Bongo Flava wakiongozwa na Madee wamemtembelea aliyekuwa Meneja wa Diamond Platnumz pamoja na Yamoto Band, Saidi Fella ‘Mkubwa Fella’ kwa lengo la kumpa salamu na kujionea hali yake ya afya kuelekea tamasha lao kubwa la miaka 30 ya Bongo Flava litakalofanyika Julai 30, 2026.
Kwa mujibu wa wasanii hao, Saidi Fella anaendelea vizuri na yupo katika hali nzuri, tofauti na baadhi ya taarifa na maneno yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Ziara hiyo imeonyesha mshikamano mkubwa miongoni mwa wadau wa muziki wa Bongo Flava, huku wasanii wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kumuombea na kumpa ushirikiano Saidi Fella.
Tamasha la maadhimisho ya miaka 30 ya Bongo Flava linatarajiwa kuwakutanisha wasanii mbalimbali wakongwe na wa kizazi kipya katika kusherehekea mafanikio na mchango wa muziki huo nchini Tanzania.
