Zanzibar, Juni 22, 2026 – Yas Fiber Tanzania itawekeza takriban shilingi bilioni 300 kwa kipindi cha miaka 20 ili kupanua huduma za intaneti yenye kasi visiwani Zanzibar kufuatia kusainiwa kwa makubaliano ya Ushirikiano kati ya kati ya Shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA), Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar na Yas Fiber.
Uwekezaji huo unatarajiwa kuwezesha huduma za mkonga wa mawasiliano (fiber) katika kuzifikia takriban kaya 100,000 katika visiwa vya Unguja na Pemba ndani ya miaka mitatu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi.
Makubaliano hayo yanaashiria hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha miundombinu ya kidigitali Zanzibar na kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti za uhakika, nafuu na zenye kasi kwa kaya, biashara, taasisi za elimu, vituo vya afya na taasisi za Serikali. Aidha, yanaunga mkono azma ya Zanzibar ya kujiimarisha kama kitovu cha ubunifu, uwekezaji na huduma za kidigitali.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Miundombinu ya kidigitali ni msingi wa uchumi wa kisasa. Ushirikiano huu utaharakisha mageuzi ya kidigitali na kusaidia kuiweka Zanzibar katika nafasi ya kuwa miongoni mwa vinara wa uchumi wa kidigitali katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Mhe. Soraga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, alisema makubaliano hayo yataongeza kasi ya upanuzi wa huduma ya mkonga wa mawasiliano visiwani humo na kusaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi.
“Ushirikiano huu utawezesha wananchi na taasisi nyingi zaidi kupata huduma za intaneti yenye kasi na kuchangia ujenzi wa miundombinu ya kidigitali inayohitajika kwa maendeleo ya Zanzibar ya sasa na ya baadae,” alisema Mhandisi Suleiman.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas Fiber, Maxime Woimant, alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya kampuni hiyo katika kuunga mkono ajenda ya mageuzi ya kidigitali nchini na maendeleo jumuishi kupitia mawasiliano ya kisasa.
“Huu ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa miundombinu ya kidigitali kuwahi kufanyika Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni. Kupitia ushirikiano huu, tutapanua upatikanaji wa huduma za intaneti za viwango vya kimataifa zitakazowezesha biashara kukua, wanafunzi kujifunza, ubunifu kwa taasisi na jamii kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali,” alisema Woimant.
Aliongeza kuwa Yas Fiber inajiona si mwekezaji pekee bali mshirika wa maendeleo wa muda mrefu anayelenga kupanua fursa za kijamii na kiuchumi kupitia mawasiliano ya uhakika na ya kisasa.
Mradi huo utatekelezwa chini ya mfumo wa Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ukiunganisha maono ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga uchumi wa kidigitali na uzoefu wa Yas Fiber katika kubuni, kuwekeza, kujenga, kuendesha na kusimamia huduma ya Fiber-to-the-Home (FTTH).
Upatikanaji bora wa huduma za intaneti unatarajiwa kuchochea ubunifu, ujasiriamali, elimu ya kidigitali, huduma za serikali mtandao (e-Government) na utoaji wa huduma za afya za kisasa, huku ukiimarisha zaidi mvuto wa Zanzibar kama kitovu cha uwekezaji, utalii na biashara katika ukanda huu.
Serikali ya Zanzibar kupitia Shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) itatoa ushirikiano katika masuala ya upatikanaji wa maeneo ya utekelezaji, uratibu wa kikanuni na usimamizi wa mradi ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa.
Mbali na uwekezaji wa miundombinu, ushirikiano huo pia utachangia maendeleo ya ujuzi wa kidigitali, uhamishaji wa maarifa na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani, hatua itakayosaidia kuandaa kizazi kijacho kushindana katika uchumi unaoendeshwa na teknolojia na kuunga mkono maono ya muda mrefu ya Zanzibar ya kuwa kitovu kinachoongoza kwa uchumi wa kidigitali Afrika Mashariki.