
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameonya kuwa atachukua hatua zozote atakazoona zinafaa iwapo Iran haitatekeleza makubaliano mapya yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili kufuatia mazungumzo yaliyofanyika nchini Uswisi.
Akizungumza katika Ofisi ya Oval Ikulu ya White House, Trump alisema kuwa Iran inalazimika kuheshimu makubaliano hayo mapya ya siku 60 yanayolenga kupunguza mvutano na kuimarisha usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.
“Iwapo Iran haitazingatia makubaliano yake au haitakuwa na mwenendo unaokubalika, nitafanya kile ninachopaswa kufanya,” alisema Trump.
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mazungumzo hayo yamezaa makubaliano ya kuanzisha hatua za kuzuia migongano na mawasiliano yasiyo sahihi katika Mlango wa Hormuz, pamoja na kuundwa kwa kitengo maalum cha uratibu kitakachosaidia kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran, yakiwemo maeneo ya Lebanon.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alisema pia kuwa Iran imekubali kuwaruhusu wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kurejea nchini humo kwa ajili ya ukaguzi wa shughuli za nyuklia. Hata hivyo, Iran imekuwa ikikanusha baadhi ya madai hayo ya Marekani kuhusu kiwango cha makubaliano yaliyofikiwa.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social Jumanne, Trump alidai kuwa Iran imekubali ukaguzi wa kiwango cha juu kabisa wa nyuklia kwa muda mrefu sana ujao.
Trump alisema hatua hiyo ni mafanikio makubwa ambayo yatahakikisha kile alichokiita uaminifu wa nyuklia na kwamba bila makubaliano hayo, mazungumzo yasingeendelea.
Rais huyo pia alitangaza kuwa kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz bila vizuizi vya kijeshi vya majini, huku akisisitiza kuwa meli za Marekani zitaendelea kuwepo eneo hilo ikiwa kutahitajika kurejesha hatua za usalama siku zijazo.
Aidha, Trump alisema fedha na nafuu ya baadhi ya vikwazo vya kiuchumi vitakavyotolewa kwa Iran vitawekwa chini ya mfumo wa escrow unaosimamiwa na Marekani, ambapo fedha hizo zitatumika kununua chakula na vifaa vya matibabu kutoka Marekani pekee.
“Mazungumzo yanaendelea vizuri,” alisema Trump, akiongeza kuwa msaada huo unalenga kukabiliana na kile alichokiita mgogoro wa kibinadamu unaoikabili Iran kwa sasa.