
Na Hosea – Manyara
Mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minane amefariki dunia huku watu wengine wawili wakinusurika kifo katika tukio linalodaiwa kusababishwa na moshi wa jiko la mkaa lililokuwa limewashwa ndani ya chumba walichokuwa wakiishi.
Tukio hilo limetokea Juni 21, 2026 katika Mtaa wa Mji Mpya, Kata ya Bagara, Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, na kuzua hofu miongoni mwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtoto huyo pamoja na watu wengine wawili walikutwa wakiwa katika hali mbaya kabla ya kubainika kuwa mtoto huyo alikuwa amefariki dunia, huku wengine wakipatiwa msaada wa haraka na kunusurika.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni jiko la mkaa lililokuwa limewashwa ndani ya chumba hicho, hali iliyosababisha athari zilizohatarisha maisha ya waliokuwemo ndani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi na mazingira yaliyosababisha tukio hilo la kusikitisha.