
Oman na Iran zimekubaliana kuendeleza mazungumzo kuhusu mustakabali wa usimamizi wa shughuli za usafiri wa baharini katika Mlango wa Hormuz, ikiwemo utoaji wa huduma za baharini na gharama zinazohusiana na matumizi ya njia hiyo muhimu kwa biashara ya dunia.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumanne baada ya mazungumzo yaliyofanyika mjini Muscat, mataifa hayo mawili yalitangaza kuunda kikosi kazi cha pamoja kitakachojumuisha maafisa kutoka wizara zao za mambo ya nje ili kuendeleza majadiliano hayo. Pia yameeleza kuwa yatawashirikisha mataifa mengine ya mwambao wa Ghuba pamoja na wadau husika katika mchakato huo.
Hatua hiyo inaonekana kuwa utekelezaji wa moja ya vipengele vya makubaliano yaliyosainiwa wiki iliyopita, yanayolitaka Iran kufanya mazungumzo na Oman pamoja na nchi nyingine za Ghuba kuhusu namna ya kusimamia huduma za usafiri na urambazaji katika Mlango wa Hormuz.
Makubaliano hayo yalitangazwa kufuatia ziara ya Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, waliokutana na Sultan wa Oman, Haitham bin Tariq, na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Sayyid Badr Albusaidi.
Katika taarifa hiyo, Oman na Iran, ambazo zote zinapakana na Mlango wa Hormuz, zilisisitiza dhamira yao ya kuhakikisha meli zinapita kwa usalama katika njia hiyo kwa mujibu wa sheria za kimataifa huku zikiheshimu mamlaka ya kila taifa juu ya maji yake ya eneo.
Pia nchi hizo mbili zimeeleza azma yao ya kuhakikisha Mlango wa Hormuz unaendelea kuwa njia salama na wazi kwa usafiri wa kimataifa, huku zikihamasisha usalama wa baharini, uhuru wa urambazaji na utulivu wa kikanda.
Mlango wa Hormuz ni moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, ambapo sehemu kubwa ya mafuta yanayouzwa katika soko la kimataifa hupitia katika njia hiyo kila siku. Kutokana na umuhimu wake wa kimkakati, maendeleo yoyote yanayohusu usimamizi wake hufuatiliwa kwa karibu na mataifa pamoja na masoko ya nishati duniani.