×

Familia ya Edgar Lungu Yashinda Rufaa, Mahakama Yaruhusu Azikwe Afrika Kusini

Familia ya rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, imepata ushindi mkubwa wa kisheria baada ya Mahakama Kuu ya Rufaa ya Afrika Kusini kuamua kuwa kiongozi huyo wa zamani anaweza kuzikwa nchini humo kulingana na matakwa ya familia yake.

Uamuzi huo uliotolewa Jumanne mjini Bloemfontein umehitimisha kwa muda mmoja wa migogoro mikubwa iliyozuka baada ya kifo cha Lungu, ingawa bado haijafahamika iwapo serikali ya Zambia itakubali matokeo hayo au kuchukua hatua nyingine za kisheria.

Kwa muda mrefu, serikali ya Zambia imekuwa ikisisitiza kuwa Lungu, kama rais wa zamani wa nchi hiyo, anastahili kupewa mazishi ya kitaifa na kuzikwa nchini Zambia pamoja na viongozi wengine wa zamani katika eneo maalumu la mazishi ya marais lililopo jijini Lusaka.

Hata hivyo, familia ya marehemu ilipinga msimamo huo na kutaka mazishi yafanyike kwa faragha nchini Afrika Kusini baada ya mazungumzo kati yao na serikali kuvunjika bila kufikia mwafaka.

Mzozo huo uliingia mahakamani baada ya Mahakama Kuu ya Afrika Kusini mjini Pretoria hapo awali kuamua kuwa serikali ya Zambia ilikuwa na haki ya kuuchukua mwili wa Lungu na kumpatia mazishi ya kitaifa. Familia ya marehemu ilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Katika hatua nyingine iliyozua sintofahamu, serikali ya Zambia ilitangaza mwezi Aprili kuwa mwili wa Lungu ulikuwa tayari umekabidhiwa rasmi kwa serikali. Hata hivyo, saa chache baadaye mahakama ya Afrika Kusini ilitoa amri ya kuzuia hatua hiyo na kuagiza mwili huo urejeshwe hadi rufaa itakaposikilizwa.

Lungu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68 katika kliniki moja mjini Pretoria, Afrika Kusini, baada ya kuugua kwa muda. Kifo chake kilizua mjadala mkubwa nchini Zambia kutokana na historia ya mvutano wa kisiasa kati yake na mrithi wake, Rais Hakainde Hichilema.

Wawili hao walikuwa wapinzani wa kisiasa kwa miaka mingi kabla ya Hichilema kumshinda Lungu katika uchaguzi wa mwaka 2021.

Baada ya kifo chake, familia ya Lungu ilieleza kuwa marehemu hakutaka Rais Hichilema kuhudhuria mazishi yake wala kuwa karibu na mwili wake kwa namna yoyote, jambo ambalo lilichangia kuongezeka kwa mvutano kuhusu maandalizi ya mazishi.

Sasa macho ya wengi yanaelekezwa kwa serikali ya Zambia ili kuona kama itaheshimu uamuzi wa mahakama au kuchukua hatua nyingine katika sakata hilo ambalo limevuta hisia za wananchi ndani na nje ya Zambia.

Leave a Comment