×

Muhoozi Aagiza Kufungwa kwa NTV Uganda na Daily Monitor

Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametangaza kuwa kituo cha televisheni cha NTV Uganda na gazeti la Daily Monitor havitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake bila kibali chake, hatua iliyozua mjadala mkubwa kuhusu hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini humo.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Muhoozi alisema kuwa vyombo hivyo viwili vya habari vitafungwa kuanzia leo.

Katika ujumbe mwingine, alieleza kuwa haamini katika mfumo wa uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda na kusisitiza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuongozwa kwa kuzingatia misingi ya mapinduzi.

“Kuanzia sasa vyombo vyote vya habari vya Uganda vitafuata sheria,” aliandika Muhoozi.

Kufikia alfajiri ya Jumapili, watazamaji wa NTV Uganda na Spark TV walikumbana na skrini tupu zilizoonyesha kuwa matangazo ya vituo hivyo hayapatikani.

Aidha, shughuli za gazeti la Daily Monitor pamoja na vituo vya redio vya KFM na Dembe FM ziliathiriwa na operesheni hiyo.

Hata hivyo, hadi taarifa hii inaandikwa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), Jeshi la Polisi la Uganda na Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) havikuwa vimetoa tamko rasmi kuhusu sababu za hatua hiyo wala msingi wa kisheria uliotumika kufunga vyombo hivyo vya habari.

Kupitia mtandao wa X, Daily Monitor ilisema bado haijaelezwa ni kwa muda gani kufungwa kwa shughuli za vyombo hivyo kutaendelea.

Tukio hilo limeibua upya wasiwasi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda, ambapo taasisi mbalimbali za habari zimekuwa zikikumbwa na shinikizo na vikwazo kutoka kwa mamlaka katika utekelezaji wa majukumu yao ya kutoa taarifa kwa umma.

Leave a Comment