×

Buchosa Yashika Nafasi ya Kwanza Mkoa wa Mwanza, Yapongezwa na Halmashauri Kuu

Jimbo la Buchosa limeshika nafasi ya kwanza kati ya majimbo ya Mkoa wa Mwanza katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika mwaka jana.

Pongezi hizo zimetolewa na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mwanza katika kikao chake kilichofanyika Juni 27, ambapo Jimbo la Buchosa lilikabidhiwa cheti maalumu cha pongezi.

Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Sengerema, Adamu Itambu, amesema sambamba na kupewa cheti hicho, Jimbo la Buchosa pia limezawadiwa Sh milioni 1 kutokana na kufanya vizuri baada ya kupata zaidi ya asilimia 98.5 ya kura.

“Nawapongeza wanachama wote wa CCM Jimbo la Buchosa pamoja na Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, kwa ushindi huu wa kihistoria wa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya uchaguzi wa Rais, Ubunge na Udiwani,” amesema Itambu.

Itambu amesema cheti hicho cha pongezi pamoja na zawadi ya fedha vilikabidhiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Marco Lushinge (Simart), kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza.

Majimbo mengine yaliyofuatia katika nafasi hizo ni Sengerema, Kwimba, Misungwi, Ukerewe, Magu, Nyamagana na Ilemela.

Leave a Comment