×

ICEA LION Yamtawaza “Mfalme wa Uwanja wa Gofu” katika Maadhimisho ya Siku ya Bima

Arusha, Tanzania – Juni 27, 2026: Maadhimisho ya Siku ya Bima yamehitimishwa kwa mafanikio kupitia mashindano ya gofu ya ICEA LION King of the Course, yaliyowakutanisha wataalamu wa sekta ya bima, viongozi wa biashara na wadau mbalimbali kwa siku ya ushindani, kujenga mahusiano na kubadilishana uzoefu.

Mashindano hayo, yaliyodhaminiwa na ICEA LION General Insurance, yameonyesha dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kuunga mkono shughuli zinazokuza ushirikiano ndani ya sekta ya bima, huku yakihamasisha ushindani wenye tija na kuimarisha mahusiano ya kitaaluma.

Mchezaji Karim Jamal aliibuka mshindi wa jumla na kutwaa taji la King of the Course (Mfalme wa Uwanja wa Gofu). Kufuatia ushindi huo, amejishindia safari yenye udhamini kamili ya kuiwakilisha Tanzania katika fainali za King of the Course, zitakazofanyika Mombasa, Kenya, mwezi Oktoba mwaka huu. Mbali na tiketi hiyo, pia alikabidhiwa zawadi mbalimbali katika hafla ya utoaji wa tuzo.

Mashindano hayo yalihudhuriwa na viongozi wa ICEA LION Group, viongozi wa Taasisi ya Bima Tanzania (Insurance Institute of Tanzania – IIT) pamoja na wadau wengine kutoka sekta ya bima, jambo lililoonyesha mshikamano na dhamira ya pamoja ya kuendelea kuimarisha na kuendeleza sekta ya bima nchini.

 

Leave a Comment