
BEIRUT – Spika wa Bunge la Lebanon na mshirika wa Hezbollah, Nabih Berri, amesema makubaliano ya mfumo wa pande tatu kati ya Lebanon, Israel na Marekani hayawezi kupitishwa kwa kuwa hayalindi maslahi ya Lebanon.
Katika taarifa iliyotolewa mapema Jumatatu kupitia chama chake cha Amal Movement, Berri alisema makubaliano hayo ni ya “masharti ya kulazimishwa” badala ya kuwa makubaliano yanayohifadhi haki za Lebanon.
“Makubaliano haya hayatapita, na hayatatekelezwa katika hali yake ya sasa,” alisema Berri.
Makubaliano hayo yanalenga kufungua njia ya amani kati ya Lebanon na Israel, huku yakiiweka sharti la kuondolewa kwa majeshi ya Israel nchini Lebanon baada ya Hezbollah kuvuliwa silaha.
Wakati huo huo, Hezbollah imesisitiza kupinga makubaliano hayo na kutangaza kuwa ina haki ya kujilinda kufuatia mashambulizi kadhaa ya Israel kusini mwa Lebanon, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo.
Kupitia taarifa yake, Hezbollah ilisema mashambulizi ya Israel ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji mapigano ambayo imekuwa ikiyaheshimu hadi sasa, na kuongeza kuwa inaendelea kufuatilia ukiukaji huo huku ikihifadhi haki ya kuilinda nchi na wananchi wake.