×

Katibu Mkuu wa CHAUMMA Akubali Kuchunguzwa, Ajiondoa Ofisini Kwa Hiari

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim.

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, ametangaza kujiondoa kwa muda katika majukumu yake ya ofisi ili kutoa nafasi kwa uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka zinazomkabili.

Katika barua aliyomwandikia Mwenyekiti wa Taifa wa CHAUMMA, Hashim Rungwe, leo Jumanne, Juni 30, 2026, Mwalim amesema uamuzi huo unalenga kuwezesha uchunguzi huru kufuatia tuhuma zilizowasilishwa mbele ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Juni 29, 2026, jijini Dar es Salaam.

Mwalim amesema yuko tayari kushirikiana kikamilifu na timu ya uchunguzi itakayoundwa na chama, pamoja na kutoa ufafanuzi wa hoja zote zitakazobainika dhidi yake. Ameongeza kuwa yuko tayari kuwajibika endapo uchunguzi utathibitisha tuhuma hizo.

“Nakuandikia barua hii kama rejea rasmi ya ombi langu mbele ya kikao cha Kamati Kuu cha Juni 29, 2026, jijini Dar es Salaam, kuhusu Kamati Kuu kuunda timu ya kuchunguza yaliyosemwa kwenye kikao na baadhi ya wajumbe kunihusu mimi, na kwamba kama nilivyotamka nitakuwa tayari kujibu yale yatakayothibitika na hata kuwajibika nayo,” ameandika Mwalim katika barua hiyo.

Aidha, katika barua hiyo, Mwalim ambaye alikuwa mgombea wa urais kupitia CHAUMMA katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ameomba kuwa kwa kipindi chote atakachokuwa nje ya ofisi, majukumu ya Katibu Mkuu yakaimishwe na Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA Tanzania Bara, Benson Kigaila, hadi uchunguzi utakapokamilika.

MAHOJIANO KUTOKA INDIA: RHODA ASIMULIA ALIVYOTAKA KUUAWA KWA KISU na BOSI WAKE – MATESO – ALIA…

Leave a Comment