
WASHINGTON, Marekani – Mahakama Kuu ya Marekani imekataa jaribio la Rais wa Marekani, Donald Trump, la kuondoa haki ya uraia wa kuzaliwa kwa watoto wanaozaliwa nchini humo na wazazi wasio na nyaraka halali za uhamiaji.
Katika uamuzi wake, majaji wengi wa Mahakama Kuu walikataa kubatilisha tafsiri ya muda mrefu ya Katiba ya Marekani ambayo imekuwa ikitambua haki ya uraia kwa watoto wanaozaliwa nchini humo, bila kujali hadhi ya uhamiaji ya wazazi wao.
Trump na timu yake ya wanasheria walikuwa wamewasilisha hoja wakitaka haki hiyo iondolewe, wakidai inaleta changamoto katika udhibiti wa uhamiaji. Hata hivyo, hoja hiyo haikupata uungwaji mkono wa kutosha kutoka kwa wataalamu wengi wa sheria na watunga sera.
Uamuzi huo unadumisha msimamo wa mahakama uliowekwa takriban miaka 150 iliyopita, na unaonekana kuwa pigo kwa ajenda ya Trump ya kuimarisha sera za uhamiaji.
Baada ya kushindwa mahakamani, wachambuzi wanaamini utawala wa Trump unaweza kuelekeza nguvu zake katika kuzuia wahamiaji wasiokuwa na nyaraka kuingia Marekani, badala ya kubadili sheria za uraia wa kuzaliwa.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa sheria, ikiwa wahamiaji hao hawataingia nchini Marekani, suala la uraia wa watoto wao wanaozaliwa nchini humo halitajitokeza.