
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kutekeleza mageuzi ya sera, sheria, kanuni na mifumo ya utoaji huduma ili kuimarisha mazingira ya biashara, uwekezaji na viwanda nchini, kwa lengo la kuiwezesha sekta binafsi kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Mwigulu amesema hayo Jumanne Juni 30, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Mwaka 2026 lililoandaliwa na Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imejipanga kuondokana na mfumo wa kudhibiti biashara na badala yake kujenga mfumo unaowezesha biashara kukua kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji, kupunguza urasimu, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuongeza ufanisi wa taasisi zinazohudumia wafanyabiashara na wawekezaji.

“Ajenda ya sekta binafsi ni ajenda ya Taifa. Hatuwezi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 bila sekta binafsi yenye nguvu, inayowezeshwa na inayoshirikiana kwa karibu na Serikali,” amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kupokea na kufanyia kazi mapendekezo kutoka sekta binafsi yenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara, kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Pia amesisitiza kuwa amani, utulivu na mshikamano wa Taifa ni msingi muhimu wa maendeleo ya uchumi, akiwataka Watanzania kuendelea kuvilinda ili kuwezesha biashara, uwekezaji na shughuli za uzalishaji kustawi.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira rafiki ya biashara kwa kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi, kukuza matumizi ya teknolojia na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa mtazamo wa kuwezesha biashara badala ya kuikwamisha.
