×

Haaland Aizamisha Ivory Coast, Norway Kukiwasha na Brazil 16 Bora

ARLINGTON, Texas: Nyota wa Norway, Erling Haaland, alifunga bao la ushindi dakika za mwisho na kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ivory Coast, na kufuzu hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia 2026 ambapo sasa itakutana na Brazil.

Mshambuliaji huyo wa Manchester City alifunga bao la ushindi dakika ya 86 kwa kumalizia krosi ya Patrick Berg, akiandika bao lake la tano kwenye mashindano hayo na kuipa Norway ushindi wake wa kwanza kabisa katika hatua ya mtoano wa Kombe la Dunia.

Norway ilianza vyema baada ya Antonio Nusa kufunga bao la kuongoza dakika ya 39 kwa shuti la kuvutia lililotinga moja kwa moja kwenye kona ya juu ya lango kufuatia pasi ya nahodha Martin Odegaard.

Ivory Coast walirejea mchezoni kipindi cha pili kupitia Amad Diallo, ambaye aliingia akitokea benchi na kusawazisha dakika ya 74 baada ya kuwapita mabeki wawili wa Norway na kufunga bao zuri lililowapa matumaini ya kusonga mbele.

Hata hivyo, matumaini hayo yalidumu kwa muda mfupi baada ya Haaland kufunga bao la ushindi dakika nne kabla ya muda wa kawaida kumalizika.

Dakika za nyongeza, Ivory Coast walikaribia kusawazisha kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Diallo, lakini kipa Orjan Nyland aliokoa kwa ustadi mkubwa na kuhakikisha Norway inalinda ushindi wake.

Ushindi huo unaifanya Norway kufuzu hatua inayofuata kwa mara ya kwanza katika historia yake ya Kombe la Dunia, huku sasa ikijiandaa kuvaana na mabingwa mara tano wa dunia, Brazil, katika mchezo utakaochezwa Jumapili mjini New Jersey.

Kwa upande wa Ivory Coast, safari yao ya Kombe la Dunia imefikia tamati licha ya kuonyesha kiwango kizuri, hasa katika kipindi cha pili ambapo waliisumbua sana safu ya ulinzi ya Norway.

Leave a Comment