×

TAKUKURU Ruvuma Yafanya Tathmini ya Miradi 290, Kesi 20 za Rushwa Zafunguliwa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Ruvuma, TAKUKURU, imefanya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kikilenga kuangalia mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizojitokeza katika usimamizi wa miradi ya maendeleo mkoani humo.

Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na viongozi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma pamoja na watendaji mbalimbali wa serikali, huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda, amesema lengo la tathmini hiyo ni kutoa mrejesho wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kusimamia matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa ubora unaostahili bila kuwepo mianya ya rushwa.

Kamanda Mwenda amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, TAKUKURU ilifuatilia jumla ya miradi 290 ambapo miradi 102 haikuwa na viashiria vya rushwa, huku miradi 188 ikibainika kuwa na viashiria hivyo. Amesema kati ya miradi hiyo, miradi 43 ilifanyiwa uchunguzi na kesi 20 zilifunguliwa mahakamani.

Aidha, amesema taasisi hiyo ilitoa maelekezo na mapendekezo ya maboresho katika miradi yote 188 iliyobainika kuwa na changamoto, huku wadau wa miradi yote 290 wakijengewa uwezo kuhusu usimamizi bora wa miradi na mapambano dhidi ya rushwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, ameipongeza TAKUKURU kwa kazi kubwa inayofanya katika kulinda rasilimali za umma na kuwataka watumishi wa serikali katika idara mbalimbali kutumia matokeo ya tathmini hiyo kujirekebisha, kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuendelea kulinda maendeleo ya sasa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

 

Leave a Comment