
Uongozi wa JKT Tanzania FC umetoa pole na kuomba radhi kufuatia kuumia kwa mshambuliaji wa Yanga SC, Pacome Zouzoua, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya JKT Tanzania na Yanga uliochezwa Juni 30, 2025, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na klabu hiyo, JKT Tanzania imesema tukio lililosababisha Zouzoua kuumia lilitokana na mchezaji wake, Hassan Wahabi, wakati wakiwania mpira, na kusisitiza kuwa halikuwa la kimakusudi.
Klabu hiyo imeeleza kuwa, kwa niaba ya Hassan Wahabi, inaomba radhi kwa tukio hilo, ikibainisha kuwa majeraha aliyoyapata Zouzoua pia yamesababisha maumivu ya kisaikolojia kwa mchezaji huyo wa JKT Tanzania.
Aidha, JKT Tanzania imemtakia Pacome Zouzoua nafuu ya haraka, ikimuombea apone na kurejea uwanjani haraka ili aendelee kucheza katika kiwango chake cha kawaida.
