×

Kifo cha Dereva wa John Heche Chachunguzwa na Polisi, Chadema Wafunguka – Video

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Amani Golugwa kimetoa taarifa za kifo cha Suez Dani Maradufu, aliyekuwa dereva wa Makamu wa Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Suez amekutwa amefariki dunia asubuhi ya leo, Jumatano, Julai 1, 2026, akiwa chumbani katika nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia mjini Kigoma.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwili wa marehemu umechukuliwa na Jeshi la Polisi na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya uchunguzi na taratibu nyingine zinazohitajika.

CHADEMA imetoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wanachama wa chama hicho kufuatia msiba huo mzito na kueleza kuwa kitaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo kadiri uchunguzi unavyoendelea na taarifa zitakavyokuwa zinapatikana.

Baada ya kupata taarifa hizo, Global TV imemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu ambaye amesema amepata taarifa kuwa kuna dereva amefariki dunia akiwa gesti ingawa bado hajajua ni dereva wa nani na kueleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea na utakapokamilika, atatoa taarifa kwa umma.

Leave a Comment