×

Airtel Yakabidhi Serikali Gawio La Sh Bilioni 65.48, Yafikisha Sh Bilioni 350 Tangu 2019

Juni, 30, 2026. Dar es Salaam. Kampuni ya Airtel Tanzania imekabidhi Serikali gawio la Sh bilioni 65.48 kwa mwaka wa fedha 2025/26, na kufikisha jumla ya gawio ililolipa Serikali tangu mwaka 2019 hadi Sh bilioni 350.

Gawio hilo lilikabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan Juni 30, 2026, Ikulu, jijini Dar es Salaam, likitokana na umiliki wa Serikali wa asilimia 49 katika Airtel Tanzania PLC.

Malipo hayo yanaifanya Airtel Tanzania kuendelea kuwa kampuni pekee binafsi ya mawasiliano nchini inayolipa gawio kwa Serikali mfululizo tangu mwaka 2019, hatua inayodhihirisha mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na mchango wa kampuni hiyo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya sekta ya kidijitali.

Akizungumza baada ya kukabidhi hundi ya gawio hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania PLC, Eliud Sanga, alisema gawio hilo ni matokeo ya uwekezaji endelevu, usimamizi madhubuti wa biashara na misingi ya utawala bora.

“Malipo haya yanaonesha kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unaweza kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa Taifa. Mbali na kutoa gawio, Airtel Tanzania inaendelea kuwekeza katika huduma zinazowawezesha Watanzania kufanya biashara, kupata taarifa, kujifunza na kuwasiliana kwa urahisi kupitia teknolojia,” alisema.

Alisema thamani ya uwekezaji haipimwi kwa faida pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi, kupanua fursa za kiuchumi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema gawio hilo linaakisi mafanikio ya kifedha ya kampuni pamoja na imani ambayo mamilioni ya Watanzania wameendelea kuiweka katika huduma zake.

“Tunajivunia kukabidhi Serikali gawio la Sh bilioni 65.48. Huu ni mchango unaotokana na imani ya wateja wetu na dhamira yetu ya kuendelea kuzalisha thamani kwa wanahisa wote,” alisema Kamoto.

Alisema Airtel Tanzania inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya huduma za intaneti, mawasiliano na ujumuishaji wa huduma za kifedha nchini.

“Leo mawasiliano si anasa tena, bali ni msingi wa ukuaji wa uchumi, elimu, ubunifu na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za maendeleo,” alisema.

Kamoto alisema kati ya mwaka 2021 na 2025, Airtel Tanzania imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 316 katika upanuzi na uboreshaji wa mtandao wake, ikiwemo huduma za 4G, 5G, Home Broadband na miundombinu ya fibre.

Aliongeza kuwa kupitia Airtel Money, kampuni hiyo inaendelea kuwawezesha mamilioni ya Watanzania kupata huduma za kutuma na kupokea fedha, kufanya malipo, kuweka akiba, kupata bima na huduma nyingine za kifedha kwa kutumia simu za mkononi.

Airtel Tanzania, kwa mujibu wa Kamoto, itaendelea kuwekeza katika teknolojia na ubunifu ili kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Leave a Comment