
Marekani imefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bosnia na Herzegovina katika mchezo wa hatua ya makundi uliochezwa mjini Santa Clara, California.
Mshambuliaji Folarin Balogun aliwapa wenyeji bao la kuongoza katika dakika ya 45 baada ya kumalizia vizuri pasi iliyotengenezwa na Malik Tillman, bao lililowapa Marekani faida muhimu kabla ya mapumziko.
Bosnia ilianza mchezo kwa kasi na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga kupitia nahodha wake mkongwe Edin Džeko na Ermedin Demirović, lakini kipa Matt Freese alifanya kazi kubwa kuokoa hatari na kuifanya Marekani ibaki salama.
Kipindi cha pili kilianza kwa pigo kwa Bosnia baada ya Džeko kushindwa kuendelea na mchezo kutokana na majeraha, hali iliyomlazimu kocha Sergej Barbarez kufanya mabadiliko ya haraka ili kuimarisha kikosi chake.

Dakika ya 64, Marekani ilipata pigo kubwa baada ya Balogun kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia ukaguzi wa VAR, uliobaini alimkanyaga Tarik Muharemović katika pambano la kuwania mpira.
Licha ya kucheza wakiwa na wachezaji 10, kikosi cha kocha Mauricio Pochettino hakikuyumba. Bosnia iliongeza presha kutafuta bao la kusawazisha, lakini safu ya ulinzi ya Marekani ilisimama imara huku kipa Freese akiendelea kuokoa hatari.
Dakika ya 82, Malik Tillman aliondoa kabisa matumaini ya Bosnia baada ya kufunga bao la pili kwa mkwaju maridadi wa faulo uliomshinda kipa Nikola Vasilj na kuifanya Marekani kuongoza kwa mabao 2-0.
Bosnia ilijaribu kusaka bao la kufutia machozi katika dakika za nyongeza, lakini haikuweza kuipenya ngome ya Marekani iliyokuwa ikicheza kwa nidhamu licha ya upungufu wa mchezaji mmoja.
Ushindi huo unaifanya Marekani kufuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia kwa ushindi wake wa kwanza wa hatua ya mtoano katika kipindi cha takribani miaka 25, huku sasa ikijiandaa kuvaana na Ubelgiji katika mchezo wa hatua ya 16 bora utakaopigwa jijini Seattle.
Kwa upande wa Balogun, licha ya kuwa shujaa kwa kufunga bao la kwanza, atakumbukwa pia kwa kadi nyekundu iliyomfanya amalize mchezo mapema na kuiacha timu yake ikipambana kwa dakika za mwisho ikiwa pungufu uwanjani.