
Switzerland imeandika historia kwa kuvunja ukame wa miaka 88 wa kushinda mchezo wa hatua ya mtoano wa Kombe la Dunia baada ya kuifunga Algeria mabao 2-0 na kutinga hatua ya 16 bora.
Ushindi huo uliopatikana jijini Vancouver ulihitimisha rekodi mbaya ya Uswisi, ambao walikuwa wameondolewa katika michezo yao saba mfululizo ya hatua za mtoano za Kombe la Dunia.
Mshambuliaji Breel Embolo aliifungia Uswisi bao la kwanza mapema dakika ya 10 kabla ya nyota wa Nottingham Forest, Dan Ndoye, kuongeza la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili dakika ya 46 na kuzima matumaini ya Algeria.
Algeria walianza mchezo kwa kasi na kuonyesha dalili za kuleta ushindani, lakini walishindwa kutumia nafasi walizopata huku safu ya ulinzi ya Uswisi ikimdhibiti vyema nahodha wao Riyad Mahrez ambaye hakufanikiwa kuleta madhara makubwa langoni mwa wapinzani.
Uswisi walipata nafasi nyingine ya kuongeza idadi ya mabao mwishoni mwa mchezo, lakini mchezaji wa akiba Fabian Rieder alishindwa kufunga akiwa katika nafasi nzuri.
Kwa ushindi huo, kikosi cha kocha Murat Yakin kimefuzu hatua ya 16 bora ambapo kitacheza dhidi ya mshindi wa mchezo kati ya Colombia na Ghana.