×

Dkt. Mwigulu: Serikali Kuboresha Upatikanaji Wa Mikopo Kwa Vijana

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaandaa maboresho ya kisera na kisheria yatakayowaondolea vijana wajasiriamali kikwazo cha muda mrefu cha ukosefu wa dhamana za mikopo kwa kuimarisha mfumo wa udhamini wa mikopo na kuruhusu matumizi ya dhamana zinazohamishika.

Amesema hayo Jumapili, Julai 5, 2026 alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya fainali za Shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026 na utoaji wa tuzo kwa washindi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mwigulu alisema mojawapo ya changamoto kubwa zinazowakabili vijana wajasiriamali si ukosefu wa mitaji pekee, bali ukosefu wa dhamana zinazokubalika na taasisi za fedha ili kuwawezesha kupata mikopo ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji.

Alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tayari ina dirisha la udhamini wa mikopo kwa biashara ndogo, za kati na kubwa, ambalo linaendelea kuboreshwa na litabadilishwa kuwa taasisi maalum itakayoratibu masuala ya udhamini wa mikopo nchini.

“Tayari kuna zaidi ya shilingi bilioni 280 kwa ajili ya jukumu hilo, na wadau wengine wameonesha nia ya kushiriki kwa kiwango cha zaidi ya dola za Marekani milioni 150. Hizi zitasaidia biashara ndogo, za kati na biashara kubwa kupata udhamini wa mikopo,” alisema Dkt. Mwigulu.

Aidha, Waziri Mkuu alisema Serikali inakusudia kupeleka Bungeni sheria itakayoruhusu matumizi ya dhamana zinazohamishika, hatua itakayowezesha wananchi wengi zaidi, hususan vijana, kupata mikopo bila kutegemea ardhi au majengo pekee.

“Tunataka kuhalalisha matumizi ya dhamana zinazohamishika. Kwa mfano, mkulima au mfugaji anayetumia stakabadhi ghalani aweze kuitumia hiyo kupata mkopo wa pembejeo bila kusubiri kuuza mazao yake,” alisema.

Leave a Comment