
Jeshi la Polisi Tanzania limefichua kuwepo kwa mipango ya siri ya vikundi vya watu wachache wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu, vifo kwa viongozi na wananchi, pamoja na mpango wa kushambulia askari ili kupora silaha kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi.
Katika taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa Jumapili, Julai 5, 2026 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, onyo kali limetolewa kwa mtu au kikundi chochote kisithubutu kushiriki katika njama hizo, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa tayari baadhi ya watu waliohusika na uratibu wa matukio hayo wameshakamatwa na uchunguzi unaendelea ili kuwafikisha mahakamani. Ufuatiliaji wa kina umebaini kuwa watu hao wamekuwa wakihamasishana kupitia mitandao na klabu za majadiliano mtandaoni.
Msemaji wa Polisi amefafanua kuwa vikundi hivyo vimekuwa vikitumia kigezo cha “haki ya kuandamana” kama kisingizio cha kutaka kutekeleza uhalifu huo, huku wakijua wazi kuwa maandamano hayo hayajafuata taratibu zilizowekwa na kisheria na kiusalama nchini. Jeshi limesema viashiria hivyo havitaweza kuvumiliwa katika nchi yoyote ile duniani.
Licha ya vitisho hivyo, Jeshi la Polisi limewahakikishia Watanzania kuwa hali ya usalama nchini kote ni shwari kabisa. Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wameimarisha ulinzi maeneo yote ya nchi, hususan kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba (Julai 7, 2026).
🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.