
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametembelea Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwajulia hali wagonjwa mbalimbali wanaopatiwa matibabu.
Akiwa hospitalini hapo, Rais Samia alimjulia hali Sheikh Rashid Hamad Othman, ambaye ni mlezi wa Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu.
Aidha, Rais Samia alipata taarifa kuwa katika wodi jirani alikuwapo pia mchezaji wa timu ya Yanga, Pacome Zouzoua, ambaye alipata majeraha wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Baada ya kupata taarifa hizo, Rais Samia pia alitembelea chumba chake na kumjulia hali, akimpa pole na kumtakia uponaji wa haraka kutokana na majeraha aliyoyapata uwanjani.
Ziara hiyo imeonesha mshikamano na ufuatiliaji wa karibu wa viongozi wa Serikali kwa wananchi na wanamichezo wanaokabiliwa na changamoto za kiafya.
