
Nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, amethibitisha kuwa Kombe la Dunia la FIFA 2026 litakuwa mashindano yake ya mwisho akiwa na timu ya taifa, akisema anataka kufurahia kila dakika iliyosalia akiwa amevaa jezi ya Ureno.
Akizungumza kuelekea mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Hispania, Ronaldo mwenye umri wa miaka 41 alisema, “Hili litakuwa Kombe langu la Dunia la mwisho.”
Nyota huyo, ambaye ameandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika matoleo sita tofauti ya Kombe la Dunia, alisema anaondoka akiwa na dhamira safi kutokana na mchango wake mkubwa kwa soka.

“Chochote kitakachotokea kesho, Cristiano ataondoka akiwa na dhamira safi. Sio asilimia 100, bali asilimia 1,000, kwa sababu nimetoa kila kitu katika soka,” alisema.
Ronaldo alianza kuchezea timu ya taifa ya Ureno katika Kombe la Dunia mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 21. Tangu wakati huo ameendelea kushiriki matoleo ya 2010, 2014, 2018, 2022 na 2026, akifikisha jumla ya Kombe la Dunia sita.
Safari yake imekuwa miongoni mwa zilizodumu kwa muda mrefu na zenye mafanikio makubwa katika historia ya soka la kimataifa, huku akivunja rekodi nyingi na kuwa mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea duniani.