×

Shigongo Amtembeza Mbunge wa Norway Serengeti, Ngorongoro na Zanzibar Kuitangaza Tanzania

Mbunge wa Jimbo la Buchosa,  Erick Shigongo, amemualika Mbunge wa Bunge la Norway, Himanshu Gulati, kutembelea Tanzania ili kujionea vivutio vya kipekee vya utalii vinavyopatikana nchini.

Katika ziara hiyo, viongozi hao walitembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, na baadaye kuelekea Zanzibar, ambako Gulati alipata fursa ya kushuhudia uzuri wa mazingira, wanyamapori na urithi wa kipekee wa Tanzania.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Gulati aliusifu utalii wa Tanzania na kueleza kuvutiwa kwake na utajiri wa rasilimali za asili pamoja na juhudi zinazofanywa katika kuhifadhi vivutio hivyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mbali na kutembelea maeneo ya utalii, Gulati pia alipata nafasi ya kukutana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, kwa mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano na mahusiano kati ya Tanzania na Norway.

Baada ya kumaliza ziara yake Tanzania Bara, mgeni huyo alielekea Zanzibar kuendelea kujionea vivutio vya utalii vya visiwa hivyo vinavyotambulika duniani, huku akitoa wito kwa wasafiri kutoka mataifa mbalimbali kutembelea Tanzania na kujionea uzuri wake wa kipekee.

Leave a Comment