
Jeshi la Polisi Tanzania limesema hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari, huku likiwahakikishia wananchi na wageni waliopo nchini kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda amani na usalama wa raia.
Katika taarifa iliyotolewa mchana wa Jumanne, Julai 7, 2026, Jeshi la Polisi lilisema limepokea simu nyingi kutoka kwa waandishi wa habari na wananchi waliotaka kufahamu hali ya usalama nchini.
Polisi ilieleza kuwa licha ya siku hiyo kuwa ni Sikukuu ya Sabasaba, ambapo baadhi ya wananchi wako mapumzikoni na wengine wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii, hali ya usalama imeendelea kuwa tulivu.
Jeshi hilo limesisitiza kuwa linaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha ulinzi unaimarishwa wakati wote ili kudumisha amani na utulivu nchini.
Aidha, Polisi imewataka wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kuepuka kuandaa au kusambaza taarifa za uongo, zinazochochea chuki, migawanyiko au kuchonganisha jamii.
Jeshi hilo limekumbusha kuwa kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika kunaweza kuwa kosa la jinai chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015, ikiwemo kifungu cha 16, pamoja na sheria nyingine za nchi.
Polisi imewahimiza wananchi kupata taarifa kutoka vyanzo rasmi, hususan vyombo vya ulinzi na usalama na mamlaka nyingine zinazohusika, badala ya kuamini kila taarifa inayosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
