
Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) umefungua ukurasa mpya wa maendeleo katika sekta ya kilimo, baada ya kutolewa kwa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 3.5 za Kitanzania kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Fedha hizo zinatolewa kupitia Wizara ya Fedha chini ya mradi wa Two Step Loan, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na JICA, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta ya kilimo.
Kupitia mpango huo, wakulima binafsi, vikundi vya wakulima pamoja na wakulima wadogo na wa kati watawezeshwa kupata mikopo yenye masharti nafuu ili kuwekeza katika shughuli za kilimo na kuongeza uzalishaji.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa SABASABA, Afisa Biashara kutoka TADB anayesimamia miradi ya benki hiyo, Elias Misana, amesema mradi huo utajikita katika mazao matano ya kimkakati ambayo ni mahindi, mpunga, ngano, alizeti na mazao ya bustani.
Amesema kupitia mpango huo, mkulima binafsi ataweza kupata mkopo wa hadi shilingi milioni 200, huku vikundi vya wakulima na makampuni vikifikia kiwango cha mikopo hadi shilingi bilioni 3.
Aidha, amesema wanawake na vijana wanaojihusisha na kilimo cha bustani watanufaika zaidi kupitia masharti nafuu ya mikopo, ikiwemo viwango vya chini vya riba na muda rafiki wa marejesho.

Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa JICA, Veronica Barua, amesema mradi wa Two Step Loan ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japani unaolenga kuwawezesha wakulima wadogo na wa kati kupata mitaji ya uwekezaji, hususan wale ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Amesema mpango huo unalenga kuimarisha uwezo wa wakulima kuzalisha kwa tija zaidi na kuchangia ukuaji wa sekta ya kilimo nchini.
Mradi huo ulianza kutekelezwa rasmi mwezi Juni mwaka 2025 na unatarajiwa kuendelea hadi mwaka 2029. Kupitia matawi ya TADB pamoja na benki washirika nchini kote, maelfu ya wakulima wanatarajiwa kunufaika, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa Tanzania.