WASHINGTON: Serikali ya Marekani imerejesha vikwazo dhidi ya mauzo ya mafuta ya Iran kufuatia mashambulizi yaliyolenga meli za kibiashara katika Mlango wa Hormuz, huku ikionya kuwa vitendo hivyo havikubaliki kabisa na vitakabiliwa na hatua kali.
Hatua hiyo ilitangazwa Jumanne Julai 7, 2026 baada ya meli tatu kuripotiwa kushambuliwa na makombora au vifaa visivyojulikana katika na karibu na Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa Shirika la Uingereza la Ufuatiliaji wa Biashara Baharini (UKMTO). Kufikia sasa, Iran haijatoa tamko rasmi wala hakuna aliyedai kuhusika na mashambulizi hayo.
Kutokana na uamuzi huo, bei ya mafuta duniani ilipanda kwa zaidi ya asilimia tano, huku wawekezaji wakihofia kuongezeka kwa mvutano katika moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa nishati duniani.
Mwezi uliopita, Wizara ya Fedha ya Marekani ilikuwa imetoa kibali kilichoruhusu Iran kuendelea kuuza mafuta hadi Agosti 21 kama sehemu ya makubaliano ya muda kati ya Washington na Tehran. Hata hivyo, baada ya uamuzi mpya, kipindi hicho kimefupishwa na shughuli zote zinazohusiana na mauzo hayo zinapaswa kukamilishwa ifikapo Julai 17.

Afisa mmoja wa Marekani amesema pamoja na hatua hiyo, mazungumzo kati ya Marekani na Iran kuhusu makubaliano ya kudumu bado yanaendelea kwa nia njema, licha ya mvutano mpya uliotokea.
Afisa mwingine wa Marekani, ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema dalili za awali zinaonyesha kuwa Iran huenda ilihusika katika mashambulizi dhidi ya meli tatu za kibiashara zilizokuwa zikisafiri katika eneo la Hormuz.
Mlango wa Hormuz, uliopo kati ya Iran na Oman, ni moja ya njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa mafuta na gesi asilia. Kabla ya kuzuka kwa mzozo huo, takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia inayosafirishwa duniani ilipitia katika njia hiyo kila siku.
Wachambuzi wanaonya kuwa iwapo hali ya usalama itaendelea kuzorota, bei za mafuta zinaweza kuendelea kupanda na kuongeza gharama za nishati kwa watumiaji na serikali duniani.
Mauzo ya mafuta yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya fedha za kigeni kwa Iran, licha ya miaka mingi ya vikwazo vya Marekani. Sehemu kubwa ya mafuta hayo huuzwa nchini China, jambo linalofanya biashara hiyo kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Iran.
Rais wa kampuni ya uchambuzi wa masoko ya nishati ya Rapidan Energy Group, Bob McNally, amesema matukio hayo yanaonyesha kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran hayana uthabiti kama ambavyo soko la mafuta lilikuwa limeamini, hivyo kuongeza hatari ya kuyumba kwa bei za mafuta katika kipindi kijacho.
