×

Rais Samia Apongeza Hatua ya Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uungwana haupaswi kuzaa kiburi wala kutoweka nafasi ya kusikilizana, akisisitiza kuwa matarajio makubwa ya wananchi ni kuona nchi ikiendelea kuwa na amani, utulivu na mshikamano.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo alipohudhuria hafla ya kushuhudia utiaji saini wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa kati ya vyama vya siasa Zanzibar, iliyofanyika katika Ikulu ya Zanzibar.

Amesema maridhiano, mazungumzo na kuheshimiana ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye umoja na maendeleo, huku akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi badala ya tofauti zao za kisiasa.

Kauli ya Rais Samia imekuja katika hafla inayotajwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha maelewano ya kisiasa na kudumisha amani nchini, hususan Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye picha na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman baada ya kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi kufuatia Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar tarehe 09 Julai, 2026.


Leave a Comment