
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva na CEO wa Konde Music Worldwide, Harmonize, ameibua hisia usiku wa kuamkia leo Julai 10, 2026 katika Hoteli ya Serena, hafla ya Look Like Money, baada ya kuonyesha ukaribu wake na staa wa filamu Bongo, Kajala Masanja, mbele ya wageni waliohudhuria.
Hafla hiyo haikuwa ya mitindo pekee, bali pia ilijaa burudani na matukio yaliyovutia wengi, huku kitendo cha Harmonize na Kajala kuwa pamoja kikitawala mazungumzo ya waliohudhuria na mashabiki mitandaoni.
Tukio hilo liliwafanya wengi kutoa maoni yao, huku baadhi ya mashabiki wakisema, “Kupendwa raha ukipata anayekupenda.” Ukaribu wao uliongeza ladha ya usiku huo na kuwa miongoni mwa matukio yaliyozungumziwa zaidi.

Kilichovutia zaidi ni pale Harmonize alipomsogelea Kajala, akamshika mkono na kuanza kucheza naye kwa muda. Kajala alionekana mtulivu wakati wa tukio hilo, hali iliyozua mijadala mbalimbali kuhusu uhusiano wao.
Muonekano wao pamoja umeongeza msisimko kwa mashabiki, hasa baada ya hivi karibuni kuibuka tetesi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwezekano wa kutengana kwao kutokana na madai ya usaliti yaliyokuwa yakihusishwa na Harmonize.
Hata hivyo, taarifa hizo zimeendelea kuwa ni mjadala wa mashabiki na wadadisi wa mambo ya burudani, kwani wawili hao hawajatoa kauli rasmi kuhusu hali ya uhusiano wao.
