
Israel imeishirikisha Marekani taarifa za kijasusi kuhusu mpango mpya na maalum unaodaiwa kuandaliwa na Iran wa kumuua Rais wa Marekani, Donald Trump, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.
Taarifa hizo zimeibuka wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiongezeka tena, huku mashambulizi mapya kutoka pande hizo yakizua hofu ya kurejea kwa vita vikubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo kama CNN na The Wall Street Journal, Marekani imekuwa ikifuatilia kwa muda mrefu taarifa kuhusu vitisho vinavyolenga kumuondoa Trump, lakini taarifa iliyotolewa na Israel imeelezwa kuwa ni mpya na inahusu mpango maalum.
Ripoti hizo zinasema maafisa wa Marekani wamepokea taarifa za kijasusi kuhusu kile kinachoelezwa kuwa mpango mpya wa Iran, ingawa hakuna maelezo ya wazi yaliyotolewa kuhusu wahusika au namna mpango huo ulivyopangwa.
Mvutano kati ya Trump na Iran umechochewa zaidi na tukio la Januari 2020, ambapo Trump, akiwa rais katika kipindi chake cha kwanza, aliidhinisha shambulio la Marekani lililomuua Jenerali wa Iran, Qassem Soleimani, hatua iliyozua hasira kubwa nchini Iran.

Iran imekuwa ikitoa kauli za kulipiza kisasi tangu tukio hilo.
Akizungumzia madai hayo akiwa ndani ya ndege ya serikali alipokuwa akirejea kutoka mkutano wa NATO, Trump alisema:
“Wanataka kumuondoa kiongozi wa Marekani — mimi. Niko kwenye orodha zao zote.”
Wakati huo huo, hatua ya Trump kubadilisha ndege yake ya safari baada ya mkutano wa NATO nchini Uturuki pia ilizua mjadala mkubwa. Badala ya kutumia ndege mpya aliyokuwa amepewa na Qatar, Trump alitumia ndege yake ya zamani ya Air Force One kutoka Uturuki kabla ya kubadilisha ndege nchini Uingereza kuelekea Washington.
Baadhi ya watu walihusisha mabadiliko hayo na masuala ya usalama, hasa kutokana na mvutano mpya na Iran. Hata hivyo, taarifa za The New York Times zilisema mabadiliko hayo yalifanywa kwa ombi la Huduma ya Ulinzi wa Rais wa Marekani (Secret Service) kama tahadhari ya kiusalama.
Trump hakutoa maelezo ya moja kwa moja kuhusu usalama wake alipoulizwa na waandishi wa habari, lakini alirejea madai ya awali kuhusu vitisho vya mauaji vinavyodaiwa kuhusishwa na Iran.
Hadi sasa, serikali ya Iran haijatoa kauli rasmi kuhusu madai haya.