
Kutokuwepo hadharani kwa Kiongozi Mkuu mpya wa Iran, Mojtaba Khamenei, kumeendelea kuzua maswali ndani na nje ya nchi huku baadhi ya wananchi wakieleza wasiwasi kuhusu uongozi wa taifa hilo katika kipindi kinachoendelea kuwa na changamoto za kiusalama na kisiasa.
Mojtaba Khamenei hajulikani alipo tangu alipoteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Iran kufuatia kifo cha baba yake, Ayatollah Ali Khamenei, aliyefariki mwishoni mwa Februari baada ya shambulio lililoripotiwa.
Kutokuwepo kwake kulionekana wazi wakati wa shughuli za mazishi ya baba yake, ambapo hakuhudhuria hadharani wala kutoa ujumbe wa maandishi au wa video, jambo lililozua mjadala kuhusu hali yake ya afya na namna anavyoongoza taifa.
Kwa mujibu wa vyanzo vya ngazi za juu vilivyonukuliwa na Reuters, Mojtaba Khamenei alipata majeraha, yakiwemo ya usoni, wakati wa shambulio lililomuua baba yake. Vyanzo hivyo vinadai kuwa anaendelea kufanya maamuzi muhimu ya serikali akiwa mbali na macho ya umma, lakini bado hajapona vya kutosha kuonekana hadharani.

Hali hiyo imezidi kuibua wasiwasi baada ya mvutano kati ya Iran na Marekani kuongezeka tena wiki hii.
Baadhi ya wananchi wa Iran waliozungumza na Reuters wamesema, licha ya sababu za kiusalama, taifa linahitaji kumuona kiongozi wake ili kurejesha imani na kuonyesha kuwa serikali inaendelea kufanya kazi ipasavyo.
Wakati wa mazishi ya Ayatollah Ali Khamenei, sala maalumu ziliongozwa na wanawe wengine watatu, huku mjukuu wa mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, Ali Khomeini, akitarajiwa kumwakilisha Mojtaba katika shughuli za maombolezo.
Tangu kuteuliwa kwake Machi 8, 2026, hakuna picha mpya, video wala hotuba ya Mojtaba Khamenei iliyotolewa rasmi kwa umma.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, alisema mwezi Mei kuwa alikutana na kiongozi huyo na kwamba hali yake ya afya ilikuwa inaendelea kuimarika.
Wachambuzi wa siasa wanasema kutokuwepo kwa Kiongozi Mkuu hadharani kwa muda mrefu kunaweza kuathiri taswira ya uongozi wa Iran, hasa wakati taifa hilo likikabiliwa na changamoto za kiusalama, uchumi unaokandamizwa na vikwazo vya kimataifa pamoja na mvutano wa kisiasa.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi zinazoonyesha kuwa Mojtaba Khamenei ameshindwa kutekeleza majukumu yake, huku mamlaka za Iran zikiendelea kusisitiza kuwa uongozi wa nchi unaendelea kama kawaida.