
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, anatarajiwa kufanya ziara nchini Oman leo Jumamosi kwa ajili ya mazungumzo yanayohusu Mlango wa Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz) na usalama wa usafiri wa meli katika njia hiyo muhimu ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran (IRNA), msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, amesema mazungumzo hayo ni mwendelezo wa mashauriano ambayo Iran na Oman wamekuwa wakiyafanya katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni.
Baghaei amesema ajenda kuu ya ziara hiyo ni kujadili hali ya Mlango wa Hormuz pamoja na kuhakikisha usalama wa meli zinazopita katika njia hiyo.
Mlango wa Hormuz ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, ambapo takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia inayouzwa katika soko la dunia hupitia eneo hilo.
Eneo hilo limeendelea kuwa chanzo cha mvutano kati ya Iran na Marekani, hasa baada ya kuzuka kwa vita kati ya Iran, Marekani na Israel mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.
Ingawa vita hivyo vilisitishwa kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa Aprili 8, bado kumekuwa na matukio ya mvutano yanayohusishwa na matumizi na udhibiti wa Mlango wa Hormuz.
Iran imeendelea kusisitiza kuwa inapaswa kuwa na udhibiti mkubwa wa njia hiyo ya kimkakati, huku ikieleza nia ya kutoza ada kwa meli zinazopita katika eneo hilo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Mlango wa Hormuz unajumuisha maji ya Iran na Oman, lakini nchi hizo hazina mamlaka ya kuzuia meli kupita au kutoza ushuru kwa njia hiyo kwa ujumla.
Ziara ya Araghchi nchini Oman inatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano na kutafuta suluhisho kuhusu matumizi salama ya mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara duniani.