×

Mjasiriamali Lilian Mmari Ajizawadia Apartment ya Milioni 400 Akitimiza Miaka 40 – Video

Mjasiriamali maarufu Lilian Mmari, anayefahamika pia kupitia LIM Microfinance, ameendelea kuonyesha kuwa malengo yanaweza kutimia kwa juhudi na nidhamu, baada ya kujizawadia apartment yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 400 ikiwa ni sehemu ya kusherehekea kutimiza umri wa miaka 40.

Mwaka mmoja uliopita, Lilian alitikisa mitandao ya kijamii baada ya kujinunulia nyumba ya kifahari ya thamani ya mabilioni alipokuwa akisherehekea miaka 39 ya kuzaliwa kwake, jambo lililovutia hisia za wengi.

Safari hii, akizungumza na Global TV, Lilian amesema mafanikio yake yametokana na kufanya kazi kwa bidii, kuwa na maono makubwa na kuamini katika ndoto zake. Amesisitiza kuwa kila mtu anaweza kufikia mafanikio ikiwa atakuwa na malengo na kuyafanyia kazi kwa kujituma.

Aidha, amekanusha vikali madai ya baadhi ya watu wanaodai kuwa mafanikio yake yanahusishwa na nguvu za giza, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi, maarifa na uvumilivu katika safari yake ya ujasiriamali.

Kauli yake imeibua mjadala mtandaoni, huku wengi wakimpongeza kwa hatua hiyo na kuona mafanikio yake kama chanzo cha motisha kwa wanawake na vijana wanaotamani kufanikiwa kupitia biashara na ujasiriamali.

Leave a Comment