
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Marekani itaendelea na mashambulizi dhidi ya Iran na kutangaza kuwa moja ya maeneo yanayolengwa ni eneo la kijeshi la Pickaxe Mountain, lililopo karibu na kituo cha nyuklia cha Natanz nchini Iran.
Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha The Hugh Hewitt Show, Trump alisema Marekani inalifuatilia kwa karibu eneo hilo na huenda likawa miongoni mwa maeneo yatakayoshambuliwa hivi karibuni.
“Tutalishambulia Pickaxe Mountain. Waambieni Wairani wawe tayari,” alisema Trump.
Trump alidai kuwa Marekani imekuwa ikifuatilia shughuli zinazohusiana na mpango wa nyuklia wa Iran na kwamba Marekani itaendelea kuchukua hatua kila inapohisi kuna tishio.
Pickaxe Mountain ni eneo lenye ulinzi mkubwa karibu na kituo cha urutubishaji madini ya urani cha Natanz, likiwa na mifumo ya mahandaki yaliyojengwa chini kabisa ya ardhi. Wataalamu wa kijeshi wanaeleza kuwa eneo hilo limeimarishwa kiasi kwamba linaweza kuwa gumu kufikiwa hata kwa baadhi ya mabomu makubwa ya kuvunja ngome yanayotumiwa na Marekani.
Kauli ya Trump imekuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka, baada ya pande hizo mbili kubadilishana mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani.
Awali Trump alisema Marekani inarejesha vizuizi dhidi ya meli za Iran katika eneo la Ghuba na kwamba Mlango wa Hormuz utaendelea kuwa wazi kwa masharti ya ada ya ulinzi itakayolipwa na meli zitakazopita.
Rais huyo ameahidi kuwa Marekani itaendelea kuishinikiza Iran kijeshi, akisema mashambulizi mapya yataendelea katika siku zinazofuata.