×

Bakwata Yawasimamisha Kazi Masheikh Watatu wa Mikoa, Yumo Sheikh Walid wa Dar

Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limewasimamisha kazi masheikh watatu wa mikoa baada ya kubaini kuwa mwenendo wao unadaiwa kwenda kinyume na misingi ya uongozi wa baraza hilo.

Uamuzi huo umefikiwa leo, Jumanne, Julai 14, 2026, katika kikao cha dharura cha Baraza la Ulamaa kilichoongozwa na Kaimu Mufti wa Tanzania ambaye pia ni Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ali Ngeruko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya kikao hicho, waliosimamishwa ni Sheikh Walid Kawambwa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Issa Nasor wa Mkoa wa Singida na Sheikh Hassan Kiburwa wa Mkoa wa Kigoma.

Baraza la Ulamaa limeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni mienendo inayokiuka misingi ya uongozi wa kibaraza, hivyo kuhitaji hatua za kinidhamu wakati taratibu nyingine zikiendelea.

“Kikao cha dharura cha Baraza la Ulamaa kimeazimia kumsimamisha Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na mienendo inayokiuka misingi ya uongozi ya kibaraza,” sehemu ya taarifa hiyo ilieleza.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua kwa undani vitendo vinavyodaiwa kufanywa na masheikh hao, wala haikueleza muda wa kusimamishwa kwao au hatua nyingine zitakazofuata.

Leave a Comment