×

Rubio azindua kampeni ya kupinga Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema serikali ya Marekani imeanzisha kampeni ya kupinga Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akidai kuwa mahakama hiyo inahatarisha mamlaka ya Marekani kwa kuwaruhusu wanajeshi na maafisa wake kufunguliwa mashtaka.

Rubio amesema Washington itafanya juhudi za kuzishawishi nchi washirika wake kukataa mamlaka ya ICC, akisisitiza kuwa Marekani haitakubali raia wake kushtakiwa na mahakama hiyo.

Aidha, ameonya kuwa mataifa yatakayoendelea kuiunga mkono ICC yanaweza kukabiliwa na hatua mbalimbali kutoka Marekani, ikiwemo vikwazo vya kiuchumi, masharti magumu ya utoaji wa visa pamoja na marufuku za kusafiri.

Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa ikipinga mamlaka ya ICC dhidi ya raia wake, ikieleza kuwa haifungwi na Mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo kwa kuwa si mwanachama wake.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa sheria za kimataifa wamekosoa msimamo huo wa Washington, wakisema ICC hailengi Marekani pekee bali ina jukumu la kushughulikia watuhumiwa wa uhalifu mkubwa wa kimataifa bila kujali uraia wao. Wameonya kuwa juhudi za kuidhoofisha mahakama hiyo zinaweza kudhoofisha uwajibikaji wa kimataifa katika kesi za uhalifu wa kivita, mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilianzishwa mwaka 2002 kupitia Mkataba wa Roma, ikiwa na dhamira ya kuwafikisha mbele ya sheria watu wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa ya kimataifa pale ambapo mifumo ya mahakama za kitaifa haiwezi au haiko tayari kuchukua hatua.

Leave a Comment