×

Miaka 50 ya SABASABA: Vodacom Yadhihirisha Mageuzi ya kidigitali nchini Tanzania

DAR ES SALAAM: Vodacom Tanzania Plc imehitimisha ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (SABASABA) kwa kuonyesha mchango wake katika kuchochea mageuzi ya kidijitali nchini, huku ikitambuliwa kwa kutunukiwa tuzo mbili muhimu kutokana na ushiriki na mchango wake katika kufanikisha maonesho hayo.

Katika maonesho hayo yaliyofanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, Vodacom iliwasilisha suluhisho mbalimbali za kidijitali zinazolenga kuboresha maisha ya Watanzania na kukuza uchumi wa kidijitali, ikiwemo huduma za fedha, afya, elimu pamoja na mifumo ya kidijitali inayowezesha biashara ndogo na za kati kutumia teknolojia katika kuendesha shughuli zao.

Kupitia jukwaa la SABASABA, Vodacom ilionesha namna ubunifu wa kiteknolojia unavyoweza kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa urahisi zaidi, kuongeza fursa za kiuchumi na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali nchini.

Baada ya kufungwa kwa maonesho hayo, Vodacom Tanzania Plc ilitambuliwa rasmi kama mshirika muhimu wa SABASABA 2026 baada ya kutunukiwa Tuzo ya Nafasi ya Tatu kwa Mshindi wa Jumla wa Maonesho pamoja na Tuzo ya Nafasi ya Pili ya Udhamini.

Katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, na Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Latifa Khamis, walipiga picha ya pamoja na wawakilishi wa kampuni mbalimbali zilizoshiriki, akiwemo Mkuu wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania Plc, Happiness Shuma.

Tuzo hizo zimekuwa ishara ya kutambua mchango wa Vodacom katika kuunga mkono maendeleo ya biashara, teknolojia na ubunifu nchini, huku kampuni hiyo ikiendelea kusisitiza dhamira yake ya kuleta suluhisho za kidijitali zinazowanufaisha wananchi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali.

Kupitia uwekezaji wake katika teknolojia na huduma bunifu, Vodacom Tanzania inaendelea kuwa sehemu muhimu ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali na matumizi mapana ya teknolojia katika maisha ya kila siku.

Leave a Comment