×

Netanyahu Atoa Onyo Kali kwa Iran “Tutalipiza Kisasi Mara Mbili”

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameonya kuwa nchi yake italipiza kisasi kwa “nguvu zaidi” iwapo itashambuliwa tena na Iran, akisema Israel haitakaa kimya dhidi ya vitisho kutoka Tehran.

Katika ujumbe wa video uliowekwa kwenye mitandao yake ya kijamii, Netanyahu aliwaambia viongozi wa Iran kuwa wasitarajie Israel kubaki bila kuchukua hatua endapo itashambuliwa.

“Msitegemee tutasalia kimya mkitushambulia,” alisema Netanyahu.

Ameongeza kuwa majibu ya Israel wakati mwingine ujao hayatakuwa sawa na mashambulizi ya awali, akidai kuwa nchi yake iko tayari kuchukua hatua kubwa zaidi kuliko ilivyowahi kufanya.

“Siku za kupigwa na kusalia kimya zimepita, tutalipiza kisasi mara mbili,” alisema.

Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Israel na Iran ukiendelea kuongezeka, huku pande hizo mbili zikiwa zimewahi kushambuliana kwa makombora na mashambulizi ya anga katika kipindi cha hivi karibuni.

Watu saba wauawa katika shambulio la Israel Gaza

Wakati huo huo, watu saba wameuawa, akiwemo afisa mkuu wa polisi, katika shambulio la anga la Israel dhidi ya kituo cha polisi kinachodhibitiwa na Hamas katika eneo la Jabalia kaskazini mwa Gaza.

Kwa mujibu wa maafisa wa afya na polisi, shambulio hilo lililenga kituo kilichokuwa karibu na soko lenye shughuli nyingi.

Mashuhuda waliiambia BBC kuwa ndege isiyo na rubani ya Israel ilirusha makombora manne katika eneo hilo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imesema Mkuu wa kituo cha polisi cha Jabalia, Kanali Mohammed Marwan Salem, pamoja na maafisa wengine walikuwa miongoni mwa waliouawa, ikitaja tukio hilo kama “mauaji”.

Mvutano huo unaendelea huku juhudi za kidiplomasia zikifanyika kutafuta njia ya kupunguza mapigano na kurejesha utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Leave a Comment