×

Urithi wa Mkapa Watajwa Kuwa Chachu ya Ushirikiano Katika Sekta ya Afya

Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imesema itaendelea kuwekeza katika teknolojia na kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali ili kuimarisha huduma za afya nchini, ikiwa ni sehemu ya kuuenzi urithi wa Hayati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa.

Akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Hayati Benjamin Mkapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Yas Tanzania alisema urithi wa Mkapa unaendelea kuishi kupitia taasisi imara, ushirikiano na uwekezaji katika mifumo inayochochea maendeleo ya wananchi.

Alisema Serikali imeitambua teknolojia kama nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuboresha mifumo ya afya, usimamizi wa taarifa za afya, huduma za kidijitali na kufanya maamuzi yanayotegemea takwimu sahihi.

Kwa mujibu wa Yas, matumizi ya teknolojia tayari yameleta mafanikio makubwa katika sekta ya afya kupitia huduma za tiba kwa njia ya mtandao (telemedicine), uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia teknolojia za kidijitali, mafunzo endelevu kwa wataalamu wa afya pamoja na huduma za dharura zinazowafikia wananchi kwa haraka zaidi.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Yas imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 1.2 katika upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwemo mtandao wa 4G na 5G ili kuhakikisha teknolojia za kisasa zinawafikia Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, alisema maendeleo ya teknolojia yamefungua fursa kwa vijana wabunifu, wahandisi na wajasiriamali wa kijamii kushiriki katika kutafuta suluhisho za changamoto zinazoikabili sekta ya afya.

Akitoa mifano ya ushirikiano ambao Yas imeufanya, alisema kampuni hiyo ilishirikiana na Serikali kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na UNICEF kuimarisha mfumo wa usajili wa vizazi kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa kutumia teknolojia ya simu, hatua iliyowezesha zaidi ya watoto milioni 13 kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa kupitia huduma za SMS.

Pia alisema Yas ilishirikiana na Hospitali ya CCBRT kusaidia matibabu ya watoto wenye tatizo la miguu ya kupinda (clubfoot), huku ikiendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya macho bila malipo Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo zaidi ya Watanzania 23,000 wamenufaika.

Kwa upande mwingine, Yas ilitangaza kuwa ipo katika mazungumzo na Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa lengo la kuanzisha ushirikiano wa kimkakati utakaolenga kuendeleza miradi endelevu ya afya na maendeleo kwa wanawake, watoto na vijana nchini.

Yas ilisisitiza kuwa itaendelea kuwa mshirika wa maendeleo kwa kuwekeza katika suluhisho bunifu za teknolojia zitakazoboresha huduma za afya, kuimarisha mifumo ya afya na kuwawezesha vijana kushiriki katika kuleta mageuzi ya sekta hiyo, ikiwa ni njia ya kuendeleza na kuuenzi urithi wa Hayati Rais Benjamin William Mkapa.

Leave a Comment