×

Iran Yadai Kushambulia Kituo cha Marekani Syria, Yatoa Tishio Jipya Hormuz

Iran kupitia Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) imedai kuwa imefanya shambulio dhidi ya kile ilichokitaja kuwa kituo cha operesheni maalumu za jeshi la Marekani katika eneo la al-Tanf, Syria, ikiwa ni kulipiza kisasi kwa kuuawa kwa wanajeshi wa Iran mjini Iranshahr, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran.

Hata hivyo, Reuters haikuweza kuthibitisha madai hayo kwa njia huru, huku serikali ya Syria na jeshi la Marekani zikiwa hazijatoa tamko la haraka kuhusu tukio hilo.

Kwa mujibu wa jeshi la Marekani, mwezi Februari lilikamilisha kuondoa wanajeshi wake kutoka kambi ya al-Tanf, iliyokuwa katika eneo la mpakani linalounganisha Syria, Jordan na Iraq.

Tangu kuongezeka kwa mvutano wa kikanda, Syria imekuwa ikijitahidi kuepuka kuhusishwa na migogoro inayozikumba nchi jirani, ikiwemo Lebanon ambako Hezbollah imekuwa ikipambana na Israel, pamoja na Iraq ambako makundi yenye uhusiano na Iran yamekuwa yakifanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora.

Rais wa Syria, Ahmed Al-Sharaa, alisema mwezi Machi kuwa nchi yake haitajiingiza katika vita vyovyote isipokuwa ikiwa itashambuliwa moja kwa moja.

“Isipokuwa Syria ishambuliwe na upande wowote, itaendelea kubaki nje ya mzozo wowote,” alinukuliwa akisema wakati wa hafla iliyoandaliwa na taasisi ya Chatham House mjini London.

Wakati huohuo, IRGC imesema Iran bado inadhibiti kikamilifu Mlango wa Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz) na kutishia kuwa hakuna mafuta wala gesi itakayoruhusiwa kupita katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji kwa muda wote ambao mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran yataendelea.

Madai hayo bado hayajathibitishwa na vyanzo huru, huku hali ya usalama Mashariki ya Kati ikiendelea kuwa ya wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa mvutano kati ya Iran na Marekani.

Leave a Comment